Friday, 27 September 2013

Ukaguzi wa miradi Ukerewe.


Picha hapo chini yaomwonesha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Injinia Evalist Ndikilo akiagana na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mwalimu Queen Mwanshinga Mlozi katika kivuko cha Ngoma kuelekea kisolya Bunda, baada ya kumaliza zoezi la ukaguzi wa miladi ya maendeleo Ukerewe. 

Yaliyojiri Miss Tanzania 2013: Nyota ya Happinness iling’ara mapema


Dar es Salaam. Suti nyeusi yenye shati nyeupe na tai nyekundu kwa wanaume na magauni marefu na mafupi kwa wanawake, ndiyo mavazi yaliyotawala usiku wa kumtafuta malkia mpya wa urembo nchini Tanzania Jumamosi iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Kila mgeni aliyewasili kwa lengo la kuingia ukumbini humo alihitajika kupita katika zulia jekundu ‘red carpet’ kwa ajili ya mahojiano mafupi na mtangazaji Sauda Mwilima wa Star Tv pia kupiga picha, kabla ya kuingia kupitia milango miwili wa VIP na ule wa viti vya kawaida.

Onyesho lilianza saa 3 usiku likifunguliwa na shoo ya warembo wote 30 waliocheza dansi kupitia wimbo wa ‘Personally’ wa wasanii P Sqare, dansi walilofunzwa na msanii wa ngoma za asili Wanne Star.

Warembo walilicheza kwa ubunifu licha ya wachache wao kukosea na kujichanganya. Katika shoo warembo hao walivalia mavazi tofauti huku wakiiga uchezaji wa Kundi la P Sqare wakichanganya na uchezaji wa wimbo wa Thriller ulioimbwa na hayati Michael Jackson.

Kikundi cha ngoma za asili cha Mama Afrika ndicho kilichoendeleza burudani katika Jukwaa la Redds Miss Tanzania lililokuwa na upana na hadhi ya aina yake ambapo baadaye warembo waliingia na mavazi ya ubunifu yaliyobuniwa na wabunifu mbalimbali wa hapa nchini.

Wakati wa kuonyesha vazi la ubunifu warembo walitambulishwa kwa majina yao na hadhi zao kwa makundi, kisha kupanda jukwaani ikishuhudiwa jitihada za wabunifu zilizoonyesha uwezo wao kwa kubuni mavazi mapya machoni pa wengi.

Baada ya kuonyesha vazi la ubunifu, warembo walirejea jukwaani safari hii wakionyesha vazi la ufukweni, lililonakshiwa na kitenge cha Kiafrika ambalo ni ubunifu wa Veronica Lugenzi. Jambo la kushangaza lililojitokeza ni vazi hilo kuvaliwa na viatu virefu, badala ya viatu vifupi vya wazi kama ilivyo uhalisia wa vazi la ufukweli, kosa linalojirudia kwa miaka kadhaa sasa.

Kuhitimishwa kwa onyesho la vazi la ufukweni kulitoa fursa kwa jukwaa kupambwa na burudani ya muziki iliyotolewa na mwanamuziki Judith Wambura maarufu Lady JD aliyevaa vazi lililopendezeshwa na mchanganyiko wa rangi nyeusi, dhahabu na fedha. Akiongozwa na Dj Choka, Lady JD aliimba wimbo unaotambulika kwa jila la Wangu aliomshirikisha Mr Blue, kisha kuimba wimbo maarufu wa Joto Hasira kabla ya kushuka jukwaani na kuwapisha warembo, waliopanda na vazi la jioni.

Licha ya awali kutangazwa kwamba mwanamuzi huyo angekuwa na bendi yake, lakini hali ilikuwa tofauti kwani aliimba kwa ‘play back’ jambo lililowashangaza wengi.

Kimbwanga kiliibuka pale mrembo mmoja aliyekuwa amevalia nambari 6 kujikuta gauni alilovaa likizuiwa na kiatu kisha kujikwaa kwenye ngazi alipotaka kupanda jukwaani kutoka nyuma ya jukwaa. Mrembo huyo alijaribu kujinasua zaidi ya mara tatu na kushindwa hivyo kuamua kurudi nyuma ya jukwaa, kabla ya kupanda tena jukwaani na kundi lililofuata huku akionekana kukosa kujiamini tofauti na alivyokuwa awali.

Baada ya warembo kuonyesha mavazi hayo walichaguliwa walioinga 15 bora sanjari na warembo watano walioshinda mataji mbalimbali.

Mwanamuziki Mike Ross kutoka Uganda ndiye aliyepokea jukwaa na kutoa burudani kabla ya kumpisha Lady JD aliyepanda kwa mara ya pili na kuuinua umati wa mashabiki kwa kuimba wimbo wake unaotamba zaidi kwa sasa ‘Yahaya’ kabla ya kumpisha jaji kusoma majina ya warembo watano walioingia hatua ya fainali.

Jaji huyo, Dk Ramesh Shaa alisoma majina ya warembo walioingia hatua ya fainali ambao ni Lucy Tomeka, Isabel Petty, Clara Bayo, Latifa Mohamed na Happiness Watimanywa.

Warembo hao waliulizwa maswali mbalimbali waliyoyachagua, wa kwanza kuchagua swali akiwa Happiness Watimanywa aliyechagua swali namba tano lilimhoji iwapo atachaguliwa kuwa Miss Tanzania atafanya kipi ambacho warembo waliotangulia walishindwa kufanya katika nyanja tofauti. Happyness alijibu swali hilo kwa ufasaha na umakini mkubwa hali iliyoufanya ukumbi ulipuke kwa shangwe.

Katika mashindano hayo ambayo kwa miaka miwili sasa yanadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s, Happiness Watimanywa, ndiye aliyeibuka kuwa malkia mpya wa urembo na kuvikwa taji la Redds Miss Tanzania, akiandika historia mpya katika miaka 21 ya mashindano hayo.

Happiness mwenye umri wa miaka 19, aliyeibukia kutoka mashindano ya urembo ngazi za vitongoji mkoani Dodoma, anakuwa mshindi wa kwanza aliyekubalika vilivyo na wapenzi wa fani ya urembo nchini sanjari na warembo wenzake 29 aliokuwa akichuana nao.

Nafasi ya pili ilikwenda kwa Latifa Mohamed huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Clara Bayo. Nafasi ya nne na tano zilikwenda kwa Isabel Petty na Lucy Tomeka.

Taji lililoongezeka usiku huo ni la Balozi wa Marie Stopes, ambalo lilikwenda kwa Marietha Boniphace.

Wasifu wa Happyness Watimanywa.
Happiness Watimanywa, ndiye msichana pekee kutoka Tanzania aliyeweka historia ya kuongoza nchi zaidi ya 150 za mtandao wa IGCSE katika somo la Uhasibu kwenye mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2010.

Yeye ni mzaliwa wa familia ya Louis Roussos ya

Morogoro. Wadogo zake Angel na Romeo sasa wanasoma shule ya St Constantine ya mkoani Arusha ambayo pia alisoma malkia huyo. Happiness amewahi kusoma Laureatte International School ya Dar es Salaam, ambapo alikutana na mwalimu wa michezo anayemtaja kwa jina la Tchalewa Ndeki akimwelezea kuwa ndiye aliyemfungulia mipaka ya kimataifa.

Akiwa Laureatte, Happiness aliwahi kwenda China na South Korea pamoja na wanafunzi wenzake katika matamasha mbalimbali ya elimu na michezo. Baada ya kumaliza kidato cha nne, alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Strathclyde cha Uingereza anaposomea Shahada ya Biashara.

Kipindi Happiness alipokuwa kwenye likizo ndefu, aliamua kujihusisha na masuala ya urembo na kufanikiwa kutwaa Taji la Miss Dodoma, Miss Kanda ya Kati na hatimaye kuingia kwenye Kambi ya Miss Tanzania.

Akiwa Miss Tanzania, Happiness alikuwa ni mshiriki wa kwanza kuingia nusu fainali ya mashindano hayo kwa kutwaa taji la Redds Miss Photogenic 2013.

Ndani ya Kambi ya Miss Tanzania, Happiness Watimanywa alikuwa mwiba kwa warembo wengine 29 wanaowania taji hilo kwani alikuwa akionyesha uwezo wa hali ya juu kuanzia kwenye kipaji hata michezo, mbali na upeo mkubwa alio nao.

Akizungumzia Redd’s Miss Tanzania, Happeness alisema kwa kifupi: “Nilipoingia kambini nilipata hofu kuona warembo wenzangu, wengi walikuwa wazuri pia wenye uwezo, nikajitahidi kuwa karibu nao kuondoa hofu na kujenga kujiamini zaidi kuwa naweza.”
Source: mwananchi. 

Nyie ni watu wabaya: Mtoto wa miaka 4 awaambia magaidi wa Alshabaab

Mtoto wa miaka minne ambaye ni raia wa Uingereza, Elliott Prior ameonyesha ushujaa wa hali ya juu baada ya kuweza kuwatolea maneno makali na ya kugusa magaidi waliovamia jengo la maduka la Westgate.
Baada ya maneno hayo, baadhi ya taarifa zilizochapishwa kwenye vyombo mbalimbali vya kimataifa, vinasema magaidi hao waliomba mtoto huyo awasamehe kwa maelezo kuwa wao siyo watu wabaya.

Inaelezwa kuwa, kitendo cha mtoto huyo kilikuwa cha kishujaa kwani aliweza kuwaeleza magaidi hao maneno hayo, bila kuogopa silaha nzito walizokuwa wameshika mkononi huku baadhi ya watu wakiwa wameshauuawa.

Mtandao wa Daily Mail unasema mtoto huyo alimwambia mmoja wa magaini hao kuwa ‘Nyie ni watu wabaya sana’.

Mtandao huo unasema mtoto huyo aliyasema maneno hayo kama njia ya kumkinga mama yake Amber, aliyekuwa amepigwa risasi mguuni pamoja na dada yake Amelie, mwenye umri wa miaka sita ambaye walikuwa wote ndani ya duka hilo.

Katika kile kilichotafsiriwa kuwa ni kuumizwa na maneno hayo, magaidi hao walimpa Elliott pamoja na dada yake mifuko miwili miwili ya chokleti na kuwaomba msamaha.

Taarifa hizo zinasema kuwa, gaidi huyo alisema “Samahani nisamehe, sisi siyo watu wabaya”.

Mama huyo anasema kuwa, kabla ya kukamatwa na magaidi hao, yeye na watoto wake walikuwa wamejificha kwenye jokofu la kuhifadhi nyama lililopo ndani ya duka la Nakumatt kwa zaidi ya saa moja na nusu. 


Anasema kuwa, baada ya kukamatwa na magaidi hayo, walimpiga risasi ya paja.


Mjomba wa watoto hao aliliambia gazeti la The Sun la Uingereza kuwa “Walikuwa na bahati kuweza kutoka kwenye mikono ya hao magaidi. Hao magaidi walisema kuwa, kama kuna mtoto yeyote aliye hai ndani ya jengo hilo wanaweza kuondoka.

‘Mama yao alisimama na kusema ‘ndio’ , binamu yangu aliweza kupata ujasiri wa kusimama na kuwaambia kuwa, nyie ni watu wabaya sana’.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, baada ya magaidi hao kujua kuwa mama huyo na watoto wake hawakuwa kati ya watu waliowalenga, hawakuwaua.


Mama huyo anasema baada ya kuwaachia  walimshawishi yeye na watoto wake kujiunga na dini ya Kiislamu wakidai kuwa, imani ya dini ya Kiisilamu haina ubaya wowote.

“Aliniambia natakiwa kubadili dini niwe Muislamu, na akaniuliza ‘unatusamehe, unatusamehe)” mama huyo aliliambia gazeti la Independent la Uingereza.

“Kwa kawaida ningesema tu chochote walichotaka ili watuachie tuondoke,” anasema mama huyo.

Baadaye magaidi hao waliwaruhusu watoto hao kutoka nje ya jengo hilo wakiwa na watoto wengine wawili akiwamo mmoja mwenye umri wa miaka 12 ambaye awali alikuwa akikataa kutoka, aking’ang’ania kwenye mwili wa mama yake ambaye alikuwa ameshafariki.

Mama wa mtoto Elliott anasema kuwa, walifanikiwa kutoka kwenye mikono ya magaidi hao kimiujiza.

Anasema kuwa, pamoja na vitu vingine walifika kwenye duka hilo ili wakanunue maziwa.

Amber anasema kuwa, magaidi hao waliwaeleza kuwa lengo lao ni kutaka kuwaua raia wa Kenya na wale wa Marekani tu.

Baadaye watoto hao walikuja kuonekana nje ya jengo hilo wakiwa wameshikilia chokleti ambazo wanadaiwa kupewa na magaidi hao, huku pembeni yao kukiwa na mwili wa mtu aliyefariki dunia.

Baba wa mtoto huyo, anasema kupona kwa familia yake kwenye tukio hilo ambalo magaidi hao waliua zaidi ya watu 62, ni muujiza wa aina yake. 


“Nashukuru sana familia yangu iko salama, nilidhani watakuwa miongoni mwa wale ambao hawakuwa na bahati,’’ Prior alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari.

‘‘Kwa sasa kama familia tunataka muda kidogo na faragha, lakini tunaomba sana wale wanaotaka kusaidia majeruhi wa tukio hili huko Kenya, watoe msaada wao kupitia Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya,” alisema.


Source: Mwananchi

Wiki ya Utalii kitaifa yafanyika jijini Mwanza

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Injinia Evarist Ndikiro akihutubia wakazi wa Mwanza