Wasema hawachukui hatua za kushughulikia kero zinazowakabili kwa muda mrefu
Wananchi wa Mtaa wa Mwanzomgumu katika Kata ya
Bigwa, Manispaa ya Morogoro, wamewashtaki kwa mbunge wa jimbo hilo,
Abdullaziz Abood, viongozi wa serikali ya mtaa huo, kwa kile
walichokielezea kuwa ni kushindwa kuwatumikia.
Wananchi hao walisema tatizo hilo pia liko katika
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, ambayo haifanyi jitihada za
kutosha, ili kuwaondolea kero mbalimbali zikiwemo kukosa baadhi ya
huduma muhimu.
Abood alipita katika mtaa huo akiwa katika ziara
yake ya kusikiliza kero za wananchi wa Kata za Bigwa, Mindu na Mkundi
ambapo pia alikabidhi vifaa mbalimbali.
Msaada wa vifaa hivyo ambao ni sehemu ya
utekelezaji wa ahadi zake za wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka
2010, ni pamoja na vyerehani, mabomba ya kusambazia maji, mawe, kokoto,
mifuko ya saruji, mchanga na hundi za fedha.
Katika hali ambayo haikutarajiwa, wananchi wa Mtaa
Mwanzomgumu, walisimamisha msafara wa mbunge Abood na kumlalamikia
kitendo cha viongozi wao kutowajali kwa maana ya kushughulikia kero zao.
Wananchi hao walisema eneo lao linakabiliwa na
matatizo mengi, lakini viongozi wao hawafanyi jitihada za kupunguza kama
si kumaliza kabisa matatizo hayo.
Walisema matatizo hayo ni pamoja na ubovu wa
barabara, kutozwa Sh100 kwa kila ndoo ya maji, ili kuchangia huduma hiyo
na kukosekana kwa kituo cha polisi.
Baada ya malalamiko hayo, Abood aliwaita viongozi
wa eneo hilo ili wajadiliane naye kuhusu namna ya kutatua matatizo hayo,
lakini waligoma.
Badala yake, walimtaka aende walikokuwa, lakini naye alikataa kwa sababu ratiba ya ziara yake ilimbana.
SOURCE: MWANANCHI.
SOURCE: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment