Friday, 15 November 2013

Pua inavyomtesa kijana Shabani

Hadithi ya kijana Waziri Shaban inatia simanzi unapoisikia. Ana matatizo makubwa ya kiafya anayohitaji msaada kutoka kwa wasamaria wema.

Dar es Salaam. Uko usemi maarufu usemao: ‘ Hujafa hujaumbika’. Kwa hakika mateso yatokanayo na matatizo ya afya ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Kwa kuwa binadamu hatujui ghaibu, yaani mambo yaliyo nje ya uwezo wa milango yetu ya fahamu, ni vigumu kutabiri hali ya maendeleo ya afya zetu.
Kimsingi, hakuna ajuaye kesho kwani hiyo ni siri ya muumba wa mbingu na ardhi. Dunia ni sawa na kitendawili.
Hadithi ya kijana Waziri Shaban inatia simanzi unapoisikia. Ana matatizo makubwa ya kiafya anayohitaji msaada kutoka kwa wasamaria wema.

Maisha tofauti
Shaban  (28) mkazi wa Gongolamboto, mkoani Dar es Salaam, anaishi maisha tofauti na ya walio wengi duniani. Yeye anapumua kwa kutumia mdomo badala ya pua kama ilivyo ada kwa wanadamu.
Hatua hiyo inatokana na ugonjwa wa nyama za pua anaosema umekuwa ukimtesa kiasi cha kujitokeza hadharani akiomba msaada kwa jamii ili hatimaye aweze kupata tiba na kuondoka na madhila hayo.
Historia ya  ugonjwa huo anasema ilianza Februari 2009, baada ya kuugua mafua makali na koo kuwasha. Alitumia dawa za kawaida bila ya mafanikio.
“Mimi nilijua ni mafua ya kawaida tu lakini kumbe sio,   kwani kila siku zilivyozidi kwenda nilianza kuona pua ikivimba kwa ndani,  jambo ambalo lilinishtua sana,” anasimulia mwanzo wa maradhi yake yanayomtesa hadi leo.
Mwaka 2010 baada ya uvimbe kujitokeza nje ya pua, alilazimika kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi. Kinyume na matarajio yake, hakupata huduma yoyote mbali ya kuelezwa awe anaripoti hapo kila baada ya miezi mitatu.
Tangu mwaka huo mpaka sasa, Shaban amekuwa akiripoti hospitalini kama anavyoeleza:  “Sikukata tamaa walivyokuwa wakiniambia kurudi kila miezi hiyo bila ya kupewa dawa ya aina yoyote,  hadi waliponiambia kuwa nitoe Sh850,000 ili nifanyiwe upasuaji.”

Ugumu anaoupata
Akizungumza kwa sauti ya mbali na taratibu, huku akitumia mdomo kupumua, anasema maradhi yake yanamweka katika wakati mgumu, kwani anashindwa hata kufanya shughuli za kumpatia riziki.
“Kama unavyojua ndugu yangu, mdomo unafanya kazi mbili; kuongea na kupumua,  hivyo siwezi hata kuongea sana kutokana na hali yangu. Nimeambiwa naweza kupona kama nitafanyiwa upasuaji,’’ anasema na kuongeza:
“ Sina ndugu wa kunisadia kwani nimezunguka sehemu mbalimbali kutafuta fedha lakini nimekosa. Najua Watanzania wenzangu wanaweza kunisaidia na kurejea katika hali yangu ya kawaida.”

Familia yake
Shaban ni baba wa mtoto mmoja. Alioa mwaka 2009 kabla ya kupatwa na maradhi hayo. Alipokuwa mzima alitimiza wajibu wote wa kuhudumia familia akiwa baba na nguzo ya familia. Hivi sasa amegeuka ombaomba, anayezunguka kwa watu wamsitiri maishani.
Anamshukuru mkewe kwa kuendelea kumvumilia hadi leo…“Unajua ukipata matatizo utashangaa kuona mwanamke anakukimbia au anakufanyia unyanyasaji, lakini mke wangu  anaendelea kunitia moyo na kuzunguka huku na huko kutafuta fedha.”
Naye mkewe anayeitwa Anna John,  anasema  hawezi kumkimbia mumewe , kwa kuwa maradhi yake ni sehemu ya majaribu ya maisha yanayoweza kumkumba mtu yeyote.
“Sitomwacha mume wangu nitahangaika naye hadi nihakikishe anapona. Ingawa  sina kazi  nitajitahidi kumtia moyo ili afarijike,’’anaeleza.
Anaamini kuwa kama maradhi hayo yamempata mume wake, yangeweza pia kumpata yeye.  Ni kwa sababu hiyo haoni sababu ya kumtekekeza mzazi mwenzake.
Kwa sasa Ana amekuwa nguzo ya famiia. Anahangaika huku na huko kutafuta chochote kwa ajili ya kuihudumia famila yake ya watu watatu.

SOURCE:MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment