*Sasa aamua kumvaa Dk Slaa, ampa masharti mazito
*Asema yeye ni binadamu, ana nyama, damu sasa amechoka
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), amesema amepokea ujumbe wa kumtishia maisha iwapo ataendelea na jitihada zake za kupambana na ufisadi.
Hata hivyo, amesema akiwa katika ziara ya Bara la Ulaya kati ya Oktoba 21 hadi Novemba 2 mwaka huu amepokea kwa njia ya barua pepe ripoti inayoitwa “Taarifa ya Siri ya Chadema” ambayo pia ilikuwa imesambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa Dar es Salaam jana Zitto “taarifa ya Chadema inasema chama hicho (chama changu), kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini mimi napokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema”.
Zitto alisema ripoti hiyo ilimhusisha pia na mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea Cordes ambaye, kwa mujibu wa ripoti hiyo, alinisaidia kupokea na kuhifadhi kiasi cha dola za Marekani 250,000 kupitia kwenye akaunti yake binafsi.
Alisema taarifa hiyo ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imemfedhehesha , kumsikitisha na kumkasirisha.
“Taarifa hii iliibuliwa katika kipindi ambacho nilikuwa safarini kutetea haki za Watanzania na Waafrika ambao utajiri wao wa rasilimali unafaidiwa na watu wachache waliohifadhi mali katika nchi za nje na pia kupigania kampuni za mataifa tajiri yalipe kodi stahiki katika nchi zetu.
“Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu,”alisema Zitto.
Aliongeza kuwa anafahamu kuwa yeye ni mwanasiasa ambaye amekuwa mlengwa wa mashambulizi kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanasiasa na vikundi vyao. “Kama mwanasiasa, niko tayari kupokea changamoto zozote zinazokuja na uanasiasa wangu”.
Hata hivyo, kitu ambacho hawezi kukubali Zitto ni kwa watu kutumia jina lake na uanasiasa wake kumchafua yeye binafsi na watu wengine wasiohusika kwa sababu ya kutaka kutimiza malengo yao ya kidhalimu.
Alifafanua kuwa raia huyo wa Kijerumani tayari amekana kuhifadhi fedha zake. Kwa maelezo yake kwa baadhi ya viongozi wa Chadema amekana kuwa na akaunti inayotajwa na amekana pia kuwepo nchini Ujerumani katika siku na wakati uliotajwa kwenye ripoti hiyo.
“Ripoti hiyo imemtaja pia mtu kama Dk.Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB ikidai nilikutana naye na alishiriki kwenye igizo hilo la kunipa fedha.
“Niseme mapema tangu kuzaliwa kwangu sijawahi hata mara moja kukutana na Dk. Kimei popote pale ndani au nje ya nchi. Kumuingiza mtu aliyejenga jina lake kwenye taaluma ya kibenki kwa sababu tu ya lengo ovu la kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si uungwana bali ni unyama,”alisisitiza.
Aliongeza kutokana na uchafuzi huu wa wazi dhidi ya taswira yake binafsi na watu wengine walioingizwa kwenye mkumbo huu, ameamua kuandika barua rasmi kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa kumwomba athibitishe kinachoitwa Taarifa ya Siri ya Chadema ni kweli ni taarifa ya chama au aikanushe ili aweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa hekaya hiyo.
“Cha ajabu, nimepokea ujumbe wa kutishiwa maisha kutoka kwa mtu(jina tunalo) na kuahidiwa kunipoteza iwapo nitaendelea na jitihada zangu za kupambana na ufisadi na kutafuta haki kwa Watanzania wote pasipo kujali tofauti zao za kiitikadi, kikanda, kikabilia na kidini,”alisema Zitto katika taarifa hiyo
Alisisitiza anatarajia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote ambao wamehusika na utungaji na uenezi wa taarifa hiyo.
“Nitahakikisha wahusika wanatafutwa na kufunguliwa mashtaka stahiki ya upotoshaji na kuchafuana.Ni matarajio yangu wale wenye mapenzi mema na Tanzania, mimi binafsi na utawala wa sheria, wataelewa nia yangu ya kutafuta haki katika suala hili,”alisema Zitto.
Hata hivyo, Zitto alisema ameamua kujitolea maisha yake kwa ajili ya Watanzania na kama alivyowahi kusema Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela;”Struggle Is My Life.”
Migogoro Chadema
Wakati huo huo Zitto amesema Chadema hakuna migogoro na kinachoonekana kuna watu wachache wasio na shughuli kuamua kuwagombanisha viongozi ndani ya chama hicho.
Zitto alitoa kauli hiyo juzi wilayani Kaliua mkoani Tabora wakati akihutubia wananachi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kolimba ambapo alitumia nafasi hiyo kueleza kinachoendelea Chadema.
Alisema kuna watu wachache hawana kazi ya kufanya na wanachokifanya sasa ni kutengeneza mazingira viongozi kugomabana na ikitokea hivyo, ndio furaha kwao.
Alifafanua kuwa mwaka 1995 kabla ya chama kuamua kukiunga mkono Chama cha NCCR Mageuzi, Edwin Mtei na Bob Makani waligombea nafasi ya kutaka kuwania uraisi ndani ya chama hicho na hakukuwa na misigano yoyote kwa kuwa walijua malengo yao ni kuwatumikia watanzania
“Hali ya watu kuwania nafasi moja ndani ya Chadema ilijirudia mwaka 1998 kwa nafasi ya uenyekiti kuwaniwa na watu wawili tofauti na hakukuwa na mgogoro,”alisema.
Aliongeza uchaguzi ndani ya chama hicho ulifanyika mwaka 2009 wakapata viongozi na kisha wakaingia kazini na kilichotokea ni kuvuna wabunge, madiwani na wenyeviti wengi.
“Sasa hali inaanza kuwa ya ajabu ajabu utafikiri kuna mtu aliyetangaza kugombea.Hatua yangu ya mwaka 2009 ilitokana na kile alichokuwa amekiona kuwa kutekeleza demokrasia ndani ya chama changu kutokana na waliomtangulia kujitokeza kuwania nafasi walizoona zinawafaa.
“Mimi ni binadamu nina damu na nyama katika umri huu mdogo nimepigwa mishale mingi sana ya kisiasa ninaumia na damu inanitoka sasa nimechoka kupigwa mishale ni lazima viongozi tuambiane ukweli na tukemee hali hii,”alisema Zitto
Hata hivyo, alisema mwanzoni hapakuwa na chama chenye nguvu kama NCCR mageuzi, lakini walipoanza kupigana kile alichokiita mishale, chama hicho kilisambaratika.
Alisema walimchafua sana Mabere kuwa yeye ni msaliti, lakini hivi sasa Marando ndio wao ndani ya Chadema na ndio mwanasheria wao , hivyo lazima waambiane ukweli.
“Viongozi tuonye haya mambo, tusipoonya tutaonekana tunashiriki na sisi, Waha tunamsemo, kwamba ‘ukiona kifaranga yupo juu ya chungu, jua mama yake yupo chini,”alisema Zitto na kushuka jukwaani.
Chadema yamjibu
Akizungumza Dar es Salaam jana kuhusu taarifa hiyo ya Zitto, Mkurugenzi wa Mawasiliano Chadema, John Mnyika alisema Zitto anaomba kitu ambacho anajua kabisa kwamba chama hicho kimefanya.
“Anajua Andrea Cordes aliniandikia email na nakala kwake na nikajibu kuwa ripoti hiyo haijaandikwa na Chadema makao makuu .
“Kikipokea malalamiko rasmi chama kitachunguza ukweli au uongo wa madai yaliyotolewa kwenye ripoti hiyo kwa sasa chama kinachukulia tu kama ripoti na habari nyingine nyingi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii mara kwa mara kuhusu Chadema na viongozi wake mbalimbali,”alisema Mnyika.
Aliongeza hata Mshauri wa masuala ya Ufundi Chadema Dk. Kitila Mkumbo anafahamu kuwa mara baada ya ripoti hiyo kuwekwa kwenye mitandao ,Naibu Katibu Mkuu Zitto alitoa kauli.
Alisema kama hakuridhika na majibu ya Zitto na kuona kulikuwa na mahitaji ya ziada anaamini Dk. Kitila anaelewa taratibu za chama angeweza tu kuwasiliana na vijana wa idara ya uenezi aliowataja kwenye andiko lake kwenye mitandao ya kijamii na idara ingetoa ufafanuzi zaidi.
“Mjadala huu usikuzwe bila sababu za msingi na kufunika masuala mengine muhimu ya kitaifa yanayoikabili nchi yetu kwa sasa.Kama kuna malalamiko yoyote yaletwe kiofisi na kwenye vikao vya chama yatashughulikiwa,”alisema Mnyika.
source. jambo leo.
No comments:
Post a Comment