Wednesday, 13 November 2013

Dk Mvungi aaga dunia

Na Mwandishi Wetu
MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyekuwa akipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini Dk. Sendongo Mvungi amefariki dunia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Assaa Rashid jana jioni  alisema Dk.Mvungi alifariki saa  8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini akiwa katika Hospitali ya Milpark.
“Kwa masikitiko makubwa,Tume inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini amefariki dunia leo(jana),”alisema.
Rashid katika taarifa yake fupi ya awali alisema :”Taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Afrika Kusini kuja nchini kwa mazishi zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa kesho(leo)”.
Marehemu Dk. Mvungi alisafirishwa siku ya Alhamisi, Novemba 7, mwaka huu kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.
Katika taarifa hiyo, Tume pia imewaomba watanzania wote kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Dk. Mvungi katika kuomboleza msiba huo.

source: jambo leo.

No comments:

Post a Comment