Monday, 25 November 2013

Rage ampinga Malinzi kweupe

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) katiba ya Simba katika mkutano alioufanya jana Jumapili kuhusu kusimamishwa kwake. Mkutano huo ulifanyika makao makuu ya klabu hiyo, Barabara ya Msimbazi, Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga. 
Na Sosthenes Nyoni, Mwananchi

Posted  Jumatatu,Novemba25  2013  saa 14:27 PM
 
Kwa ufupi
 
Awali, Rais wa TFF, Jamal Malinzi akizungumza na Wanahabari alimtaka Rage aitishe mkutano mkuu wa mabadiliko ya katiba ndani ya siku 14 kuanzia Novemba 23. 

Rage amemteua Wambura  kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage amepinga agizo la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linalomtaka aitishe mkutano wa mabadiliko ya katiba ndani ya siku 14 na kusema endapo msimamo huo utasisitizwa basi atajiuzulu.
Awali, Rais wa TFF, Jamal Malinzi akizungumza na Wanahabari alimtaka Rage aitishe mkutano mkuu wa mabadiliko ya katiba ndani ya siku 14 kuanzia Novemba 23.
“Kutokana na Mgogoro uliopo Simba hivi sasa, kamati ya utendaji ya TFF inamwagiza mwenyekiti wa Simba, Aden Rage kuitisha mkutano mkuu wa dharura ndani ya siku 14 kuanzia sasa.
“Uamuzi huu umefanywa kwa kuzingatia ibara ya 1(6) ya katiba ya Simba inayosema Simba Sports Klabu ni mwanachama wa TFF, itaheshimu katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF,” alisema Malinzi.
Lakini jana mwenyekiti wa Simba, Rage akizungumzia agizo hilo la TFF alisema hawezi kuitisha mkutano huo kwa shinikizo la shirikisho hilo.
“Katiba ya TFF ibara 31(1-5) inasema mjumbe wa kamati ya utendaji atakosa sifa kama atakosa mambo manne, ataandika barua kujiuzulu, haudhurii mikutano minne iliyoitishwa na mwenyekiti  halali, kama atakuwa mgonjwa amelala kitandani miezi 12  mgonjwa na amekutwa na kosa la jinai,” alisema Rage.
Alisema,” nimesikitishwa na agizo la TFF kunitaka niitishe  mkutano ndani ya siku 14, wamenukuu ibara ya 1(6), Simba Sports Club ni mwanachama wa TFF, nitaheshimu katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF, hatuwezi kuheshimu kuvunja katiba ya TFF, mimi naambiwa nivunje katiba ya TFF naambiwa nivunje katiba ya Simba.”
“Tena wamekwenda mbali wananitaka niitishe mkutano ndani ya siku 14 sijui wameitoa wapi, haipo kwenye katiba ya TFF wala Simba, mimi msimamo wangu kama mwenyekiti wa Simba siitishi mkutano nalindwa na katiba,” alisema Rage.
Akizungumzia kamati ya utendaji iliyoketi na kumsimamisha, Rage alisema ilikuwa batili kutokana na kuongozwa na mtu ambaye hatambuliki katika katiba ya klabu yake ya Simba.
“Kamati ya utendaji ya Simba inakamilika kwa kuwa na mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe saba waliochaguliwa katika uchaguzi halali, hakuna  sehemu inayomtaja kaimu mwenyekiti au umewahi kuona wapi mtu ana kaimu na kukaimu, huyo Itangire si amewekwa tu pale, alichaguliwa na nani?” Alihoji Rage. Alijitapa kwa kusema hatua yake ya kwenda kuzunguza makao makuu ya klabu yake imedhihirisha yeye ndiye mwanaume wa kweli na aliwaponda wapinzani wake kwamba ni waoga kutokana na kumjadili mafichoni.
“Siku zote ukitaka kupindua nchi unaanza kuteka Ikulu, mimi ndiyo mwanaume wa kweli siyo hao wanaoongelea huko uchochoroni huo si uoga?” alijigamba Rage. 
 
 Katika hatua nyingine, Rage amemteua Michael Wambura kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba na kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Rahma Al Kharoosi aliyejizulu kutokana na kutingwa na majukumu.
 
SOURSE: MWANANCHI. 

No comments:

Post a Comment