KIMATAIFA

KIMATAIFAWAZIRI MKUU ATEKWA.

WAZIRI Mkuu nchini Libya, Bw. Ali Zeidan, jana alfajiri alitekwa na watu wenye silaha katika hoteli anayoishi Mjini Tripoli nchini humo na baadaye kuachiwa huru.
Serikali ya Libya ilisema, inaamini Bw. Zeidan alitekwa na wanamgambo wa Kiislamu ambao ni kundi la waasi linaloitwa Revolutionaries Operations Room.
Ilisema kutekwa kwa Bw. Zeidan kulitokana na maagizo ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali nchini humo ingawa Wizara ya Sheria ya nchi hiyo imekanusha madai hayo.
Kundi hilo lilikuwa miongoni mwa makundi ya wapiganaji waliofurahishwa na hatua ya makomandoo wa Marekani kumkamata Anas Al-Liby ambaye ni mshukiwa wa Kundi la Kigaidi la al-Qaeda.
Makundi hayo yanapinga hatua ya Marekani kuingilia uhuru wa Taifa hilo na kutaka maelezo kutoka kwa Balozi wa Marekani nchini humo.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), lilisema Bw. Zeidan alitekwa nyara ndani ya hoteli ya kifahari anamoishi ambapo Serikali nchini humo, inakabiliwa na shinikizo kali baada ya makomando wa Marekani kumkamata kiongozi huyo.
Makomandoo wa Marekani walimkamata Liby Oktoba 5, mwaka huu, kwa madai ya kuhusika na mashambulizi ya kigaidi ambayo yalifanywa katika Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Kenya, mwaka 2008.
Oktoba 7, mwaka huu, Libya ilimuhoji Balozi wa Marekani juu ya kukamatwa Liby ambapo Bw. Zeidan alitoa wito kwa Marekani na nchi za Magharibi kuisaidia Serikali ya Libya ili kukomesha vitendo vya wapiganaji wenye itikadi kali nchini humo.
Katika mahojiano yake na BBC, Bw. Zeidan alisema Libya inatumiwa kama kambi ya kuweka silaha na kuzisafirisha kwenda maeneo mengine ya kanda hiyo.
Shirika la habari la Associated Press, lilisema zaidi ya watu 150 waliokuwa na silaha wakiwa katika magari, waliizingira hoteli anayoishi Bw. Zeidan ya Corinthia mapema alfajiri.
Wengine waliingia katika jengo hilo hadi ghorofa ya 21 ambayo anaishi Bw. Zeidan, kuwafunga pingu walinzi wake kabla ya kumkamata na kuondoka naye.
Shirika hilo lilidai Bw. Zeidan hakutoa upinzani wowote wakati akiongozwa kwenda katika magari ya watekaji hao. Meneja wa Usalama katika hoteli hiyo, Mohamed Shaaban alisema watu hao walisema agizo la kukamatwa kwake limetolewa na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali nchini humo.

No comments:

Post a Comment