Habari za Kisiasa

‘Mikopo elimu ya juu itazamwe’

na Abdallah Khamis, Tabora

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema mikopo inayotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu itazamwe upya akisema kuwa lengo lake ni kuhakikisha watoto wanaotoka katika familia masikini wananufaika nayo.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alitoa kauli hiyo juzi mkoani Tabora wakati akihutubia mikutano mbalimbali ya kuimarisha chama katika ziara yake inayoendelea kwenye Kanda ya Magharibi.
Alisema kuwa serikali imekuwa ikitoa mikopo hiyo kwa madaraja ya ufaulu pasipo kuangalia mazingira ya upatikanaji wa madaraja hayo.
Kwa mujibu wa Zitto ni ngumu kwa watoto wengi wanaotoka katika familia za kimasikini ambao kuanzia shule ya msingi wanasoma katika shule zisizo na walimu wa kutosha, vitabu vya kiada na maabara, wakaweza kupata daraja la kwanza na la pili yatakayowawezesha kupata mkopo wa kujiunga na elimu ya juu.
“Nimepigiwa simu na kijana toka Nanyumbu, Mtwara ananieleza kuwa huu ni mwaka wa pili anashindwa kuendelea na elimu ya juu licha ya kupata nafasi, huku wazazi wake wakiwa hawana fedha na serikali haimpi mkopo kwa sababu ya daraja lake la ufaulu,” alisema.
Alisisitiza kuwa wakati hali ikiwa hivyo kwa watoto wanaotoka katika familia za kimasikini, watoto wa matajiri mikopo hiyo imekuwa halali yao kwa kuwa kuanzia shule ya msingi wanakuwa wameshajengewa mazingira ya kuipata.
Katika hali ya kusikitisha, Zitto alisema anashangazwa na hekima aliyonayo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo aliyewataka wanafunzi walioshindwa kuendelea na elimu ya juu kwa kukosa mikopo wakauze ng’ombe, mbuzi na kuku kwa ajili ya kuendelea na masomo.
“Hii ni kebehi na ulevi wa madaraka kwa Watanzania, serikali inakusanya kodi inasemaje haina fedha ya kuwasomesha vijana wake? Mbona posho za kutulipa sisi pamoja na safari za rais hazikosekani?” alihoji Zitto.
Alisema ni wakati muafaka kwa mikopo inayotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu ikawa ni kwa gharama za kuishi na zile za masomo, kwamba wanafunzi wasidaiwe bali wasome bure.

Source: Tanzania Daima.

No comments:

Post a Comment