Watoto hawa ni miongoni mwa watoto wengi wanaofanya kazi za kugonga
kokoto na kuchonga matofali kisiwani Pemba. Watoto wengi wanatumikishwa
katika ajira hiyo ngumu, huku wakikosa haki yao ya kupata elimu. Picha
na Talib Ussi.
Na Talib Ussi, Mwananchi
Posted Ijumaa,Novemba15 2013 saa 11:47 AM
Posted Ijumaa,Novemba15 2013 saa 11:47 AM
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi kupitia mradi wa
kupambana na ajira ngumu kwa watoto, zaidi ya watoto 15,000
wanajishughulisha na ajira tena zile ngumu.
Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikitimiza
miaka 50 tangu Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyojenga mazingira mazuri ya
maendeleo, visiwa vya Unguja na Pemba vimeathirika na ajira ngumu
zinazowahusisha watoto.
Hicho ni kikwazo kinachoweza kuifanya Zanzibar
ishindwe kuyafikia Malengo ya Milenia, ambayo yanataka hadi kufikia
mwaka 2015 watoto wote wapate fursa na haki za msingi za elimu.
Vichocheo vya ajira kwa watoto
Kwa Zanzibar sababu ni nyingi, ikiwamo wazazi
kutokuwa na mwamko wa kuwasomesha watoto wao na kutamalaki kwa umaskini
katika familia nyingi.
Hata hivyo, wapo wazazi walioamua tu
kuwatumikisha watoto wao katika ajira ngumu, huku wakisingizia kuwa
wanafanya hivyo kwa sababu ya ugumu wa maisha.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi kupitia mradi
wa kupambana na ajira ngumu kwa watoto, zaidi ya watoto 15,000
wanajishughulisha na ajira tena zile ngumu.
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
(Tamwa) ambacho ni sehemu ya washiriki wa mradi, Sheha Haji Dau,
anasema waliwatembelea watoto zaidi ya 264 na kubaini 80 wanaishi katika
mazingira hatarishi kwa kujishughulisha na ajira ngumu.
Baada ya kuwabaini anasema wamekuwa wakihakikisha
wanarudi shule kama anavyosema: “Kijiji cha Charawe pekee watoto 16
wamerudishwa shule. Wanaendelea vizuri na masomo, huku tukitoa elimu kwa
wazazi wafuatilie maendeleo yao. ‘’
Hali mbaya Pemba
Kisiwa cha Pemba kinatajwa kuathirika zaidi kwa
kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi hata
ndani ya familia zao.
Mratibu wa asasi ya kiraia inayoshughulikia
mapambano ya ajira ngumu za watoto katika Mkoa wa Kaskazini Pemba
(Kukhawa), Mgeni Hamad Othman anasema ajira za watoto zimerudisha nyuma
maendeleo ya sekta ya elimu katika kisiwa cha Pemba.
‘Mkoa wa Kaskazini ambapo naufanyia kazi, ajira mbaya za watoto
zimetawala na kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu kwa maendeleo ya
Taifa,’’ anasema.
Hata hivyo, anashukuru kuwa kupitia mradi huo wa
miaka mitatu, wamefanikiwa kuwarudisha shule watoto 106 wanaosoma katika
shule mbalimbali.
Akitoa mfano wa watoto katika maeneo ya Mwambe,
vitongoji na Micheweni, anasema watoto wamekuwa wakifanya kazi za
kugonga kokoto na uchongaji wa matofali.
Ushuhuda
Mkazi wa Mwamba, Mcha Makame Bahani anawasimamia
watoto wapatao saba anaosema, asubuhi wanafanya kazi ya kugonga kokoto
ili wapata fedha za matumizi, kisha baadaye wanakwenda shule.
‘Ni kweli ajira za watoto kugonga kokoto zipo
Mwamba kwa wingi, lakini sababu kubwa tunakabiliwa na umaskini
uliokithiri. Hatuna ajira na Serikali haijaweka mikakati ya kutuwezesha
miradi midogo midogo,’’ anasema.
Naye mtoto Mariam Daud Hamad (16), anakiri kuwa
kugonga kokoto ndiyo kazi yake ya kila siku kuanzia asubuhi hadi jioni.
Kinachosikitisha zaidi ni kuwa Mariam hakuwahi kupelekwa shule na
wazazi.
‘Kwa siku nzima napata madebe 12 ambapo debe moja
linauzwa kwa Sh150 mimi sijapelekwa shule lakini nikipelekwa nipo tayari
kusoma,’’anaeleza.
Kwa upande wake mchuuzi katika soko la Wesha,
lililopo Chakechake, Kai Kombo Omar anasema iliwachukua miezi sita
kuwapiga marufuku wanafunzi wa shule 27 waliokuwa sokoni hapo kuparua
samaki.
‘Sisi katika soko la Wesha tumefanikiwa na
kukomesha ajira mbaya kwa watoto, kama unavyoona hakuna mtoto hapa
anayefanya kazi za kuparua samaki na kuchukuwa mizigo,’’ anaeleza.
Mratibu wa Kukhawa anasema katika utafiti
walioufanya katika Shehia moja tu ya Mwambe, watoto 280 wamebainika
kufanya kazi ngumu, ambapo asasi yake imo mbioni kuwasaidia na
kuwarudisha shule.
‘Ajira za watoto ni changamoto kubwa Pemba
kutokana na familia kukabiliwa na hali ngumu ya maisha, sasa sijuwi
itakuwaje mradi huu utakapomaliza muda wake,’’anasema.
Ofisa Mwandamizi wa asasi ya Piro, inayojihusisha na watoto
walio kwenye ajira mbaya katika Wilaya ya Micheweni, Sada Hamad Mbarouk
anasema wilaya hiyo imeathirika kwa kiasi kikubwa.
‘Wilaya ya Micheweni Pemba imeathirika na ajira
mbaya za watoto, ambapo tayari tumewafikia zaidi ya watoto 562 ambao
wamerudi shule,’’ anasema.
Watoto wanaorudishwa shule wamekuwa wakisaidiwa madaftari,viatu pamoja na vifaa vyote vya kujifunzia.
Furaha ya kurudi shule
Ali Musa anafurahi kurudi shule baada ya kipindi
kirefu cha kukacha masomo na kwenda kufanya kazi. Anasema: “Nimerudi
shule zaidi ya miezi sita sasa baada ya kutoroka, ambapo nimepokelewa
vizuri na walimu na kupata ushirikiano mkubwa.’’
Kauli ya Serikali
Waziri wa Uwezeshaji Wananchi, Wanawake, Vijana na
Watoto, Zainab Omar Mohamed , anakiri kuwepo kwa watoto
wanaotumikishwa katika ajira ngumu.
Hata hivyo, anaeleza kuwa sheria za Zanzibar na
mikataba ya kimataifa inapiga marufuku ajira hizo, ambapo wazazi
wanaobainika huchukuliwa hatua za kisheria.
‘’Serikali inapiga marufuku ajira mbaya za watoto
zenye madhara, ambazo husababisha wakose fursa mbali mbali ikiwemo
elimu. Tupo katika mikakati ya kupinga ajira hizo,’’ anasema Waziri
Mohamed.
SOURCE: MWANANCHI.
SOURCE: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment