Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki
Na Aron Msigwa – Maelezo
SERIKALI imewataka wananchi kuzitumia ipasavyo fursa
za elimu zinazotolewa kupitia programu mbalimbali, ikiwemo Elimu ya
Watu Wazima (EWW) na ile ya Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (ENMRA) ili
kupunguza tatizo la umasikini, maradhi na ujinga.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Said Meck Sadiki wakati akitoa taarifa kwa wananchi kuhusu
Maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi
yatakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 13, 2013 yakiwa na
kauli mbiu “Kisomo kwa ajili ya Karne ya 21”
Alisema Serikali imeanzisha programu anuai za elimu kuanzia msingi
mpaka sekondari kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata fursa hiyo na
kuondokana na tatizo Umaskini, maradhi na ujinga na kuwawezesha
kujikwamua kiuchumi, Kijamii, Kisiasa na Kiutamaduni. Ameeleza kuwa mkoa
wa Dar es Salaam kwa sasa unaratibu program mbalimbali zikiwemo Mpango
wa Elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA) unaowahusisha wanafunzi wenye
umri kati ya miaka 9 hadi 18 ambao husoma katika mfumo wa makundi rika.
Alisema jumla ya wanafunzi 1,846 wamejiunga na program hiyo kwa mwaka
2013 wakihusiha wale wenye umri wa miaka 9 mpaka 13 na 14 mpaka 18.
Meck Sadiki ameeleza kuwa mkoa wa Dar es Salaam pia unasimamia Mpango wa
Uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA) unaohusu utoaji
wa Elimu kupitia kisomo cha kujiendeleza na kisomo chenye manufaa
kinachowahusisha watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 18 wapatao 1,678
waliojiunga kwa mwaka 2013.
Aliongeza kuwa wanafunzi wapatao 2,309 wamejiunga na programu ya
Elimu ya Sekondari Huria (PESH) ambayo huendeshwa kwa wanafunzi ambao
wamekosa sifa za kuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari kupitia
chaguo la mfumo rasmi.
“Wanafunzi wanaosoma katika mpango wa PESH serikali imewawekea
utaratibu wa kusoma katika shule za msingi na sekondari ambazo hazina
utaratibu wa awamu mbili za kusoma, wao husoma jioni baada ya muda wa
kawaida wa masomo”
Aidha amezitaja programu nyingine za elimu zinazowahusisha watu
wazima na vijana kuwa ni pamoja na Elimu ya Masafa na Ana kwa Ana (ODL)
ambayo ina jumla ya wanafunzi 335 wanaoendelea na masomo na Elimu
Changamani (IPPE) ambayo inawahusisha vijana 112 waliomaliza elimu ya
msingi na kukosa nafasi ya kujiunga na sekondari ambao hujengewa uwezo
katika masomo ya maarifa, ufundi, afya, maktaba na mazingira.
Kuhusu maadhimisho ya mwaka huu, Mecki Sadiki ameeleza kuwa pamoja na
mambo mengine yatakuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii
kushiriki kikamilifu kusikiliza, kusoma na kutoa maoni ya upatikanaji wa
katiba mpya nchini, kuongeza mwamko kwa jamii katika masuala ya elimu,
kutathmini utekelezaji wa azimio la ulimwengu kuhusu utoaji wa elimu kwa
wote na kutathmini mafanikio na mapungufu ya utekelezaji wa Elimu ya
Watu Wazima (EWW) na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (ENMRA).
source: dar leo.
No comments:
Post a Comment