VILIO vya furaha jana vilitawala katika Mahakama Kuu Kanda ya
Mwanza baada ya aliyekuwa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza,
Leonard Bihondo na wenzake watatu kuachiwa huru katika kesi ya mauaji
ya aliyekuwa Katibu wa CCM Kata ya Isamilo, Bahati Stephan iliyokuwa
ikiwakabili.
Akisoma hukumu hiyo ya shauri namba 79 la mwaka 2011, Jaji Aisheri
Sumari alisema kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri umeshindwa
kumtia hatiani mshitakiwa namba moja katika kesi hiyo, Jumanne Oscar
ambaye alituhumiwa kutekeleza mauaji hayo kwa kumchoma Bahati kisu
katika ziwa lake la kushoto.
Akisoma maelezo ya shahidi namba 16 na 18 ambao walikuwa ni askari
polisi waliokabidhiana mtuhumiwa namba moja, alisema kuwa ushahidi wao
ulikuwa na mkanganyiko hivyo kutoa faida kwa washitakiwa.
Jaji Sumari alisema kwa maelezo yao, shahidi namba 16 anasema kuwa
alipelekwa mahabusu na shahidi namba 18 kumchukua mshitakiwa namba
moja, kisha kmpeleka kwa RCO Muna kuchukuliwa maelezo.
Aliongeza kuwa shahidi namba 18 katika ushahidi wake alisema kuwa
tangu alipomkabidhisha mtuhumiwa kwa OCD siku ya tukio, hajawahi kurudi
wa kushughulika na kesi hiyo hadi alipokwenda kutoa ushahidi
mahakamani.
“Mkanganyiko huo ulitakiwa kuondolewa na Malingumu ambaye mpaka sasa
ni askari, lakini upande wa Jamhuri wameshindwa kushughulika na hilo,
hivyo kushindwa kuamini maelezo ya ushahidi,” alisema.
Jaji Sumari alisema kuwa pande wa mashitaka haukutaka Malingumu
kufika mahakamani kuthibitisha mtuhumiwa aliyekabidhiwa na shahidi
namba 18 (Sostenas) kama ndiye mshitakiwa namba moja.
Alisema kuwa uwezekano wa kuwachanganya washitakiwa ni mkubwa
kutokana na ushahidi uliotolewa na shahidi namba 16 na 18, kwa sababu
kama mshitakiwa namba moja ndiye aliyekamatwa ziwani, haoni kwanini awe
na majeraha wakati shahidi namba 7 na namba 2 walimkabidhi mtuhumiwa
kwa askari bila majeraha yoyote.
Kufuatia maelezo hayo, Jaji Sumari alisema kuwa kuna mkanganyiko
mkubwa upande wa mashahidi wa Jamhuri juu ya mtu aliyechukuliwa na
polisi na mtuhumiwa aliyetolewa ziwani.
“Hapa kuna maswali mengi ya kujiuliza, kwanini upande wa Jamhuri
hawakuita gwaride la utambuzi kwa sababu wananchi ndio waliomkamata
mtuhumiwa ziwani na kumkabidhi kwa askari wakati kesi hiyo imechukua
muda mrefu?” alihoji.
Alisema kuwa anakubaliana na hoja za wakili wa mshitakiwa wa kwanza,
Stephan Magoiga kuwa ushahidi unaotolewa hapo ni utambuzi wa mahakamani
na si eneo la tukio ambapo mahakama haiwezi kumtia hatiani mshitakiwa
huyo.
Kuhusu upande wa utetezi wa washitakiwa, Jaji Sumari alisema kuwa
mtuhumiwa namba moja ambaye alikuwa na kesi ya kujibu aliuchambua
vizuri ushahidi uliotolewa na shahidi namba 16 na 18 na kudai kuwa
umeonyesha wazi mkanganyiko kutokana na vielelezo vya nguo ambavyo
alikuwa amevaa.
Alisema kuwa mashahidi hao walimtambua kwa suruali aliyokuwa amevaa
aina ya jinzi ambapo kielelezo kilichofikishwa mahakamani ni cha
suruali ya khaki ambayo ilikuwa na damu.
Kutokana na maelezo hayo, Jaji Sumari alisema kuwa ameridhika na
ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri kuwa hauwezi kuwatia hatiani
washitakiwa wote wanne, hivyo akawaachia huru.
Source; Tanzania daima
|
No comments:
Post a Comment