NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Zitto Kabwe amesema kuna njama inayofanywa na wabunge wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kutaka mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya usiishe
ili wajiongezee muda hadi mwaka 2017.
Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema
kuwa lengo la wabunge hao ni kutaka muda wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015
usogezwe mbele hadi 2017 ili waendelee kukaa madarakani.
Alisema kuwa CHADEMA haitakubali uvunjwaji wa aina
yoyote wa katiba, na hivyo kumtahadharisha Rais Jakaya Kikwete kutothubutu
kukubaliana na fitna hizo.
Madai ya Zitto yaliwahi pia kutolewa na Mwenyekiti wa
Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alisema kuwa CCM
wanataka kukwamisha mchakato wa katiba makusudi ili kutengeneza sababu ya
kuongeza muda wa Rais Kikwete kubaki madarakani kwa miaka miwili zaidi.
Prof. Lipumba alisema kuwa hoja ambayo CCM wanataka
kuitumia kukwamisha mchakato huo, ni muundo wa serikali ambapo dakika za
mwisho wanataka kukubali serikali tatu kisha watumie kisingizio cha
uundwaji wa taifa la Tanganyika kuchelewesha katiba mpya.
Akihutubia mikutano mbalimbali ya hadhara katika Jimbo
la Bukene mkoani hapa, ukiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya ujenzi wa chama
katika Kanda ya Magharibi jana, Zitto alisema hata vurugu zilizotokea
bungeni hivi karibuni na Naibu Spika Job Ndugai, kuruhusu askari waingie
ndani ya Bunge kuwakamata na kuwapiga wabunge wa upinzani, ilikuwa ni
sehemu ya mpango huo wa kutaka kusogezwa mbele kwa muda wa wabunge kutoka
madarakani.
Zitto alifafanua kuwa hoja inayojengwa na wabunge hao
ambao wameshaanza kuipenyeza kwa ajili ya kumfikia Rais Kikwete, ni kwamba
kama katiba mpya itapatikana kwa wakati huu, muda wa kujiandaa na uchaguzi
wa mwaka 2015 utakuwa hautoshi.
“Hawa ni wabunge waroho wa madaraka, hawajafanya jambo
lolote jema katika majimbo yao, na sasa wanajua hawawezi kurudi ndiyo maana
wanataka muda usogezwe na wao waendelee kulipwa mshahara na posho.
“Sisi CHADEMA tunasema hilo hapana, hatuwezi kukubali
uchaguzi usogezwe kwa miaka miwili, na namuonya Rais Kikwete asithubutu
kuingia katika mkenge huo unaowahusisha baadhi ya mawaziri,” alisema.
Aliongeza kuwa wananchi waliwachagua wabunge wao
kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitano, na kwamba kuwe na katiba mpya au
isiwepo ni muhimu uchaguzi kufanyika ili wale walioshindwa kuwajibika wakae
pembeni.
Zitto alisema CHADEMA inatoa kauli hiyo ili wananchi
wajue mkakati huo, na washiriki kuupigia kelele, kwa kile alichoeleza kuwa
mipango hiyo imeshaanza jijini Dar es Salaam na Dodoma.
Kwa mujibu wa Zitto, baadhi ya mawaziri wanataka kutumia
nafasi ya kuwa karibu na rais ili kumshawishi akubali mkakati huo, kwa
kumueleza kuwa hali hiyo itamjengea heshima na kumbukumbu ya kuiachia nchi
katiba iliyo bora.
Avunja ngome ya CCM
Katika hatua nyingine, Zitto ameitikisa ngome ya
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi.
Dalili ya ngome hiyo kutikiswa ilianza kuonekana mapema
wiki hii wakati viongozi wa CHADEMA Wilaya ya Uyui walipokuwa wakifanya
maandalizi ya mkutano katika Kata ya Mabama, ambako ni nyumbani kwa kigogo
huyo.
Baada ya kutangazwa kuwapo kwa mkutano wa CHADEMA katika
kata hiyo, gazeti hili lilishuhudia jitihada mbalimbali za viongozi wa CCM
zikifanyika, ikiwemo kuweka bendera mpya kila baada ya nyumba mbili, huku
zile nyumba za wakazi wasiokuwa wafuasi wa chama hicho, zikiwekwa
barabarani.
Baadhi ya wakazi wa kata hiyo na maeneo mengine ya
jirani ambao walijitokeza kumsikiliza Zitto, walieleza kuwa baadhi ya
nyumba zilizowekwa bendera wakazi wake walitishiwa kufanyiwa hujuma kupitia
ofisi ya mtendaji wa kata hiyo endapo wangekataa.
“Unaona bendera zote ni mpya, hapa tumewachoka, na sasa
wanatumia vitisho kutaka kuweka bendera zao kwenye nyumba zetu,” alisema
mmoja wa wakazi hao ambaye hakutaka kutajwa jina.
Hata hivyo, mkutano wa Zitto nusura uingie dosari baada
ya msafara wake kuchelewa kufika katika Kata ya Mabama, kisha mtu
aliyejitambulisha kama ofisa mtendaji wa kata hiyo, kuwataka wananchi
watawanyike kutoka katika uwanja wa mkutano.
Lakini wananchi hao hawakukubaliana na agizo hilo na
kuahidi kumsubiri Zitto ambaye aliwasili katika eneo la mkutano saa 12:47
jioni na kuwahutubia hadi saa moja na robo usiku.
Kabla ya kuhutubia mkutano huo, Zitto aligawa kadi kwa
wanachama wapya waliotoka CCM na kuwataka wasiogope vitisho vyovyote
vinavyofanywa na viongozi wa chama hicho.
Alisema CCM imeua njia ya reli iliyokuwa ikiwasaidia
wakazi wa Mabama kufanya shughuli za kila siku za kujipatia kipato.
Hata hivyo, Wakasuvi alikanusha chama chake kujihusisha
na vitendo vya kuwatisha wananchi, akisema kuwa wao wanatumia nguvu ya
hoja.
SOURCE: Tanzania Daima.
|
No comments:
Post a Comment